
TAMKO LA KULAANI MATUKIO YA ULAWITI KWA WATOTO NCHINI
Mnamo tarehe 16 Januari, 2023, gazeti la Nipashe lilichapisha Makala yenye kichwa cha habari kinachosema “Watoto wafundishwa kulawitiana shuleni” ndani ya Makala hiyo mwandishi ame hoji wazazi mbalimbali ambao wamekiri kuwa watoto wao ni wahanga wa vitendo vya ulawiti na unyanyasaji wa kijinsia.
Wazazi wa wahanga walieleza kuwa watoto wao wa kike na wa kiume wamekua wakifundishwa kufanya vitendo vya ulawiti katika shule wanazosoma. Kibaya zaidi wamekuwa wakifundishwa vitendo hivyo ambavyo ni uvunjifu mkubwa wa maadili na sheria za nchi yetu na walezi wao wa karibu (Patrons).
Taarifa hizi ni mwendelezo wa matukio mbalimbali ya ukatili kwa watoto ambayo yamebainika kuongezeka kwa kasi nchini. Kwa mujibu wa waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalumu, Dk Dorothy Gwajima, jumla ya matukio 1,114 ya watoto kulawitiwa yaliripotiwa kwa kipindi cha mwaka 2021 pekee. Kwa maelezo ya Waziri Dk Gwajima, watoto 5,899 waliripotiwa kubakwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja wa 2021.
Matukio haya ni kinyume na haki za binadamu huku watoto wakiwa wahanga wakubwa wa matukio hayo. Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya mwaka 1977, inatamka kuwa “watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanao haki bila ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria”. Pia ibara ya 14 ya Katiba ya nchi inasema kuwa “kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa sheria.
Kadhalika, kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto, ya Mwaka 2009, watoto wana haki ya kulindwa dhidi ya unyanyasaji na ukatili wa kila aina. Pia kifungu cha 9 (3) (a) wazazi wana wajibu wa kuwalinda watoto dhidi ya kutelekezwa, kutegwa, kufanyiwa vurugu, kunyanyaswa, kutumikishwa vibaya, na kuwa katika mazingira mabaya kimwili na kimaadili.
Kwa upande mwingine, mikataba mbalimbali ya kimataifa inayohusu haki za watoto kama vile mkataba wa kimataifa wa haki za watoto (Convention on the Rights of the Child) uliopitishwa na Baraza kuu la umoja wa mataifa tarehe 20 Novemba, 1989 linasisitiza kulindwa kwa haki za watoto.
Shirika la Mazingira, Haki za Binadamu na Jinsia (Envirocare), tunakemea na kulaani vikali vitendo hivi vya ulawiti na unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto. Tunatoa wito kwa Jeshi la polisi na serikali kwa ujumla kuchukua hatua kali za kisheria kwa watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo na hasa watakaobainika kufundisha watoto vitendo hivi visivokubalika katika jamii yetu. Pia, tunatoa rai kwa wazazi, walezi, walimu na jamii kwa ujumla kuwa makini katika malezi na makuzi ya watoto. Envirocare tunahimiza serikali na wadau wengine kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule zote kwa ajili ya kupinga ukatili wa kijinsia na namna bora ya kuweza kuripoti matukio yote ya ukatili wa kijinsia na hasa vitendo vya ulawiti na ubakaji.
Tuwalinde watoto kwani ni taifa la leo na kesho!
Imetolewa leo tarehe 20 Januari, 2023 na.
Shirika la Mazingira, Haki za Binadamu na Jinsia (Envirocare)
Loyce Lema.
Mkurugenzi Mtendaji.
